Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas
Jeshi la polisi mkoani Arusha limemuua kwa kumpiga risasi mtuhumiwa namba moja wa milipuko ya mabomu katika mikusanyiko na kuwamwagia viongozi wa dini tindikali baada ya kujaribu kutoroka akiwa chini ya ulinzi akiwa njiani kwenda kuonesha bomu alilokuwa amelificha maeneo ya Kondoa mkoani Dodoma .
Akitoa taarifa za kifo cha mtuhumiwa huyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas amesema marehemu Yahaya Hassan Omari Hela maarufu kwa jina la (Sensei) ambaye alikuwa anatafutwa kwa muda mrefu.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa wiki mbili zilizopita mkoani Morogroro na kupelekwa Arusha na bado alikuwa anaendelea kuhojiwa.
Kwa mujibu wa kamandaa Sabas mtuhumiwa marehemu Yahaya alishakiri kuwa yeye ndiye alikuwa msimamizi mkuu wa matukio yote ya milipuko ya mabomu na ya kumwagia viongozi wa dini tindikali yaliyowahi kutokea mkoani Arusha na maeneo mengine.
Aidha kamanda Sabas amefaanua kuwa baada ya marehemu mtuhumiwa kukiri tuhuma hizo alikuwa bado anaendelea kutoa ushirikiano kwa kuanza kuonesha vitendea kazi yakiwemo mabomu ambayo alidaiwa kuyaficha Kondoa mkoani Dodoma.
Amesema wakati anasafirishwa walipofika eneo la Kisongo katika barabara kuu inayoenda Dodoma majira ya usiku alifanya jaribio la kutaka kutoroka na ndipo akapigwa risasi iliyomjeruhi mguu na kiuno na akafariki wakati anapelekwa hosipitali.
Kamanda Sabas alitaja baadhi ya matukio ambayo mtuhumiwa alikiri kuhusika kuwa ni pamoja na matukio yote ya kumwagia viongozi wa dini tindikali, matukio yote ya milipuko ya mabomu likiwemo lililotokea kanisani, kwenye mkutano wa CHADEMA, baa ya Arusha Night Park na mgahawa wa Vama matukio ambayo licha ya kusababisha vifo vya watu wasio na hatia yalisababisha watu wengi kujeruhiwa.
Kamanda Sabas amewashukuru wananchi wa mkoa wa Arusha na maeneo mengine kwa kutoa ushirikiano wa kukabiliana na wimbi la uhalifu na amewaomba kuendeleza mshikamano huo