Mwili wa marehemu ukiingizwa katika Kituo cha Polisi
Katika tukio lisilo la kawaida mamia ya wananchi wa kijiji cha Kisangura wamechukua mwili wa marehemu Samson Nyakiha na kuupeleka katika kituo kikuu cha polisi cha wilaya ya Serengeti mkoani Mara baada kudai kuwa ndugu yao alifariki dunia katika hospitali ya rufaa ya Bugando kutokana na kipigo alichokipata kutoka kwa askari polisi wa wilaya hiyo kwa kushirikiana na askari wa hifadhi ya taifa ya Serengeti.
Ndugu hao wa marehemu baada ya kuchukua mwili huo katika hospitali ya rufaa ya Bugando walikwenda moja kwa moja hadi kituo cha polisi na kuingiza jeneza lenye mwili wa marehemu huyo ndani, kisha kuutelekeza na kukusanyika nje ya kituo hicho wakati wakingoja hatua ambazo zinachukuliwa na jeshi hilo kuhusu watuhumiwa hao wa mauaji.
Wakizungumza kabla ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa mara RCO Rogathe Mlasani kufika na kuzungumza na wafiwa hao, wamesikitishwa na askari hao kupiga ndugu yao na kusababisha kifo lakini wakati wote serikali imeshindwa kuchukua hatua.
Naye mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa mara RCO Rogathe Mlasani, akizungumza na wafiwa hao, pamoja na kuwapa pole, amesema jeshi la polisi chini ya ofisi yake litachukua hatua za haraka za kuchunguza tukio hilo na kwamba wahusika wote watakaobainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake wakili wa upande wa wafiwa Stephen Magoiga, amewaomba wafiwa hao kuwa watulivu wakati wakisubiri taarifa rasmi za jeshi la polisi kama ilivyoahidiwa na mkuu huyo wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Mara kuwa taarifa rasmi za uchunguzi wa tukio hilo zitatolewa ndani ya siku Saba.
Baada ya makubaliano hayo ndugu hao waliuchukua mwili huo wa marehemu na kwenda katika kijiji hicho cha kisangura kwa ajili ya mazishi.