Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya Policy Forum, Bw. Semkae Kilonzo.
Afisa ushawishi na mawasiliano kwa umma wa asasi ya Policy forum ambayo inajishughulisha na ufuatiliaji wa sera za maendeleo Bw. Alex Modest, amesema hali hiyo imebainika kufuatia utafiti uliofanywa na taasisi hiyo katika halmashauri kadhaa nchini.
Utafiti huo umefanywa kwa pamoja kati ya taasisi ya Policy Forum chuo kikuu cha nchini Afrika Kusini ambapo pamoja na mambo mengine umegundua pia mwamko mdogo wa wananchi katika kudai haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na huduma bora za elimu na afya.
Mbali ya uwajibikaji hafifu na matazamo hasi juu ya asasi za kiraia, Bw. Modest amesema taasisi hiyo imebaini pia kuwa baadhi ya sera zimekuwa haziendani na sheria za sekta husika kiasi cha kuibuka kwa mkanganyiko na ucheleweshaji katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo.
Akifafanua kuhusu mtazamo hasi, Modest amesema baadhi ya halmashauri nchini zimekuwa zikiziona asasi za kiraia kama maadui wa kile wanachokifanya na kwamba kuna haja ya watendaji wa halmashauri hizo kuachana na mtazamo huo na badala yake washirikiane na asasi za kiraia kwani lengo lao la pamoja ni kuwahudumia wananchi ambao ni Watanzania.