Saturday , 9th Jan , 2016

Watu 79 wamekamatwa na Idara ya Uhamiaji nchini kwa kosa la kuishi nchini bila vibali na kufanya kazi wasizo na taaluma nazo.

Naibu Kamishna wa Uhamiaji Dar es Salaam, John Msumule amesema watuhumiwa hao wanatoka katika nchi 15.

Nchi hizo na idadi ya wahamiaji haramu ni Nigeria (4), China (20), Ethiopia (23), Korea (9), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC (6), Somalia (3),Uganda (2), Madagascar (5), Burundi (2), Ivory Coast (1), Lebanon (1), India (1), Zimbabwe (1) na Ghana (1).

Amesema katika ‘kamata kamata’ hiyo pia wamefanikiwa kukamata Watanzania watatu, ambao wamekuwa wakijishughulisha na kukusanya, kuwahifadhi na kuwasafirisha wasichana kuwapeleka nchi za mbali, kwa ajili ya kufanya kazi mbalimbali.

“Tumewakamata wasichana sita ambao walikuwa wamekusanywa na watanzania hao ili kusafirishwa na tutawachukulia hatua za kisheria ili kutoa fundisho kwa wengine wenye nia ya kufanya mtindo kama huu,” alisema Msumule.

Aliongeza kuwa idara hiyo imewarudisha nchini mwao wahamiaji 23 raia wa Ethiopia na watuhumiwa nane wa nchi mbalimbali,wamefikishwa mahakamani. Alisema shughuli ya kuwarejesha raia wengine katika nchi zao zinaendelea.

Msumule aliwataka wamiliki wa nyumba za kulala wageni na nyumba za kupanga, wahakikishe wanatambua wateja wao ni raia wa wapi na anafanya kazi gani, kabla ya kufanya naye mkataba wa aina yoyote.

Zoezi la kamata kamata wahamiaji haramu limeanza baada ya wizara ya mambo ya ndani kutangaza oparesheni kabambe ya kuwakamata raia wote wa kigeni wanaoishi nchini wakijihusisha na kazi mbalimbali kinyume na sheria, pia wizara ilisisitiza kuwa raia wote wa kigeni wanaofanya kazi nchini ambazo zinawezafanywa na wazawa mikataba yao ikiisha waondoke nchini warejee makwao.