Thursday , 14th Jun , 2018

Rais John Magufuli atuma salamu za rambirambi kufuatia vifo vya vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 11, Askari JWTZ 1 na Dereva waliokuwa wakisafiri kutoka Tabora kwenda Mbeya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kisha kupinduka katika eneo la Mwansekwa, Mjini Mbeya.

Rais Magufuli ametuma salamu hizo kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Amos Makalla baada ya muda mchache kutokea kwa ajali hiyo leo Juni 14, 2018.

"Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya ajali ya basi la abiria la kampuni ya Igunga Trans iliyosababisha vifo vya vijana wetu 11 Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), askari 1 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na dereva waliopoteza maisha leo tarehe 14 Juni, 2018 majira ya mchana katika mteremko wa Mwansekwa uliopo Mjini Mbeya", amesema Rais Magufuli.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli ameendelea kwa kusema "tumewapoteza vijana shupavu waliojitolea kulijenga na kulipigania Taifa, nimeumizwa sana na vifo vya vijana hawa na nawapa pole Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jen. Venance Salvatory Mabeyo, Mkuu wa JKT Mej Jen. Martin Busungu, familia za marehemu na wote walioguswa na msiba huu".

Kwa upande mwingine, Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, na amewaombea majeruhi wote 25 wa ajali hiyo wapone haraka ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na majukumu ya kila siku.