Rais wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Peter Kuga Mziray.
Akizungumza kwa njia ya simu akiwa njiani kuelekea mjini Dodoma kwa ajili ya vikao vya bunge la Katiba vinavyoendelea kesho; Mziray amesema wajumbe kutoka kundi la UKAWA hawana nguvu ya kisheria ya kusimamisha mchakato huo, huku mkazi wa Dar es Salaam Bw. Hussein Mkude akitaka kuheshimiwa kwa maoni yaliyomo ndani ya rasimu ya pili ya katiba.
Kwa mujibu wa Mziray, Tanzania ina vyama zaidi ya ishirini ambavyo vimesajiliwa kihalali kufanya shughuli za kisiasa na kidemokrasia na kwamba vyama vitatu pekee ambavyo vinaunda UKAWA haviwezi kuhodhi haki ya vyama vingine vilivyosalia kushiriki mchakato wa katiba mpya.
Mziray amesema vyama vya siasa ni mmoja kati ya wadau muhimu wa mchakato wa katiba wakiwemo wananchi wasio fungamana na siasa zozote na kwamba hatua ya UKAWA kususia mchakato huo haiwazuii wadau wengine kuendelea na harakati za kuwapatia Watanzania katiba wanayoitaka.
Mziray amesema hata hivyo baraza lake limepanga kukutana na pande hasimu ndani ya bunge la katiba kwa lengo la kujadiliana ili kuondoa tofauti na mchakato huo kuendelea kama ulivyopangwa.