Tuesday , 8th Nov , 2016

Familia ya Marehemu Spika Mstaafu wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania marehemu Samwel Sitta, imesema wanatarajia kupokea mwili wa marehemu ukitokea Ujerumani siku ya Alhamis wiki hii.

Marehemu Spika mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samwel Sitta.

Taarifa hiyo imetolewa na Msemaji wa Familia Bw. Gerald Mongella wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari na kusema baada ya mwili kutolewa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwlimu Julius Nyerere mwili huo utapelekwa moja kwa moja nyumbani kwa marehemu Masaki Jijini Dar es Salaam.

Amesema siku ya Ijumaa mwili wa marehemu Sitta utapelekwa viwanja vya Karimjee kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho na baada ya hapo mwili utapelekwa mkoani Dodoma kwa ajili ya kuwapa wabunge fursa ya kutoa heshima za Kibunge.

Marehemu Samwel Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia juzi katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alipokuwa akipatiwa matibabu tangu mwezi uliopita.