Tuesday , 22nd Mar , 2016

Siku moja baada ya Mwandishi wa habari wa Gazeti la Mwananchi na Radio ya Deutch Welle, Salma Said, kupatikana akiwa hai baada ya kutekwa nyara na watu wasiojulikana hatimae amejitokeza mbele ya waandishi wa habari na kueleza kilichomsibu.

Salma Said akiwa katika Ofisi za Baraza la Habari Tanzania MCT na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Mujubi Mukajanga.

Akizungumzia tukio hilo Jijini Dar es Salaam, Salma amesema baada ya kushuka Uwanja wa Ndege alikutana gari iliyokuwa na watu aisowafahamu ambao walilazimisha kuingia kwenye gari yao na alipokataa ndipo walipomvuta na kumingiza kwenye gari kwa nguvu na kumpeleka kusikojulikana.

Bi. Salma Said amesema baada ya kufika sehemu hiyo watu hao walikuwa wakimpiga kila mara kiasi cha kumfanya kushindwa kupumua ambapo aliwaambia watamuua lakini wakamwambia lengo lao sio kumuua.

Salma amesema kuwa lengo la watu hao ilikua ni kumshikilia mpaka hapo uchaguzi wa marudio utakapopita ndio watamuachia aendelee na shughuli zake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mratibu wa Kitaifa-Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, amewataka polisi watoe taarifa ya uchunguzi waliofanya wakati mwandishi huyo alipokua anashikiliwa na watu hao.