Tuesday , 21st Jul , 2015

Mbunge wa jimbo la Kyela na waziri wa Afrika Mashariki Dr. Harrison Mwakyembe amebatizwa jina kuwa Pierre Nkuruzinza baada ya kutangaza nia ya kugombea ubunge kwa muhula wa tatu na kuwaacha wananchi wakishikwa na butwaa.

MBUNGE wa jimbo la Kyela na waziri wa Afrika Mashariki Dr,Harrison,Mwakyembe akihutubia wananchi katika mkutano wa Hadhara.

Akizungumza na chombo hiki mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Gabriel Kipija amesema mbunge huyo aliahidi kuwa ataondoka na Kikwete lakini amegeuka Nkuruzinza kwa kutaka kugombea tena kwa muhula wa tatu.

Amesema mbali na kuwa mbunge huyo anatajwa na wananchi wa Kyela kuwa ni mmoja wa wabunge mizigo na kupelekea kuzomewa kwa mabango kutokana na kulitelekeza jimbo hilo lakini bado ameonekena kuwa na roho ya paka kwa kuwania tena.

Kipija ambaye ni diwani wa kata ya Kyela kati, na mkurugenzi wa taasisi ya Keifo inayomiliki shule wilayani humo, amesema mbali na kupunguza kero zilizopo wilayani humo akiwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo lakini Mwakyembe hakushiriki vikao.

Aidha aliongeza kuwa, chama cha Mapinduzi kisipokuwa makini kumchagua kiongozi anaye kubalika watarajie kulikabidhi jimbo hilo mikononi Mwa Ukawa, na kwamba dalili za kukataliwa Dr. Mwakyembe wameziona wakilazimisha itakula kwao.