Thursday , 17th Nov , 2016

Watu sita wanaodaiwa kuwa vinara wa mtandao wa kukusanya kuuza vipande vya meno ya tembo akiwemo Yusuph Ali Yusumbu marufu kama Mpemba wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jana jijini Dar es Salaam

Watuhumiwa wakiwa mahakamani

Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne ya kuhujumu uchumi baada ya kukutwa na pembe za ndovu zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 783.

Walifikishwa mbele ya hakimu mkazi Thomas Simba na kusomewa mashtaka hayo na mwendesha mashtaka wa serikali Paul Kadushi.

Kadushi aliambia mahakama kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa manne ambapo kwa nyakati na sehemu tofauti katika mikoa ya Dar es Salaama, Morogoro, Iringa, Tanga na Mtwara wakiwa na mtu mwingine ambaye hakuwepo mahakamani hapo walikutwa na pembe za ndovu mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Yusuph Ally 'Mpemba'

Kadushi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba jamhuri inaandaa nyaraka mbalimbali ikiwemo maelezo ya mashahidi pamoja na vielelezo kwaajili ya kufikishwa katika mahakama maalum ya kesi za rushwa na uhujumu uchumi  

Kesi hiyo itatajwa tena Desemba mosi na washitakiwa wamerudishwa mahabusu.