
Mwenyekiti CCM mkoa wa Iringa ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Mbeya Mh. Albert Chalamila (aliyesimama).
Chalamila ameongea na www.eatv.tv na kuweka wazi kuwa hajaachia kofia moja kama ilivyoelezwa na badala yake anaendelea na kazi zote mbili ya ukuu wa mkoa wa Mbeya ambayo ameteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli pamoja na uenyekiti wa CCM aliyokuwa nayo kabla ya uteuzi.
''Nimeona mitandaoni lakini sijaachia kofia moja, nasubiri maelekezo ya chama kutoka kwa katibu mkuu yeye atawasiliana na katibu wa mkoa na nitafuata nitakachoambiwa lakini kwasasa naendelea na wadhifa wangu na kesho nitakuwa mkutano wa CCM mkoa wa Iringa'', amesema.
Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole suala hilo lipo chini ya kanuni ya uchaguzi ya CCM ambayo inaeleza bayana mtu mmoja kofia moja, lakini pia kanuni imetoa mamlaka kwa Kamati Kuu ya chama kumwezesha mtu mmoja kushika kofia mbili endapo itaona inafaa.
Binafsi Chalamila amesema tangu ateuliwe anaona kila kitu kinakwenda sawa tu na hajaona kama kuna sehemu inapwaya na hajaona kama inampasa kujiuzulu kabla ya kupewa utaratibu na Katibu Mkuu.