Thursday , 7th Sep , 2017

Mkuu wa mkoa wa Dodoma ndg. Jordan Rugimbana amepiga marufuku watu kwenda hospitalini kumuona Tundu Lissu kwa sababu za kiusalama na kuongeza kwamba eneo la hospitali ni finyu.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana

"Niwaombe sana wale watu wenye nia njema ya kutaka kufika hospitali  kumuona Mh. Lissu wasifanye hivyo kwani hospitali ya mkoa eneo ni finyu sana.. Msifanye mkusanyiko wowote hospitali kwani eneo haliruhusu kumpokea kila mtu, tuwe wavumilivu mpaka pale taarifa zitakapotolewa" Rugimbana.

Akizungumza na wanahabari Mh. Rugimbana amesema pia hatohitaji kuona mikusanyiko pia ndani ya Mkoa wa Dodoma kwani jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kufahamu asili ya tukio lilivyotokea hivyo kuwepo mikusanyiko kutapelekea shida ya askari kufanya kazi.

Pamoja na hayo Mkuu huyo wa mkoa  amesema tayari Naibu Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameshafika hospitalini hapo lakini madaktari wamemtaka kutofanya chochote mpaka pale atakapopatiwa maelekezo.

Kwa upande wa Daktari anayemuhudumiwa Mh. Lissu amesema kuwa Lissu amekutwa na risasi zipatazo tano katika mwili wake ambazo ni sehemu za tumboni pamoja na mguu.

Aidha amesema kuwa Madaktari wanaendelea na matibabu na kuongeza kuwa jopo la madaktari wanaomshugulikia litatoa taarifa kamili baadae juu ya mwenendo wa hali ya Lissu. Jeshi la polisi limeomba wananchi watakaokuwa na taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo kuzifikisha kwao.

"Kwenye chumba cha mgonjwa wanaopaswa kuingia ni madaktari wanaomuhudumia. Tundu Lissu yupo imara na matibabu ya awali tumekwishampatia. Majeraha ni ya tumbo,  na mguu lakini idadi ya risasi na mambo mengine tutawajulisha mamlaka husika" Mganga Mkuu hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema amesema habari za Tundu Lissu kupelekwa jijini Nairobi bado hazina ukweli wowote kwani wanasubiri ripoti ya madaktari wanaomhudumia Lissu.

Naye Kamanda wa polisi wa Dodoma Gilesi Mroto amewataka wananchi wenye taarifa zozote kuhusiana na taarifa za tukio hilo waweze kutoa ushirikiano ili kuwatia nguvuni wahalifu hao.

Ndugu Tundu Lissu amepigwa risasi muda wa Saa 7:30 mchana aliporejea nyumbani kwake 'Area D' Dodoma kwa ajili ya chakula cha mchana.