Sunday , 26th Aug , 2018

Kitengo cha Afya katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kimeweka udhibiti madhubuti wa  kujikinga na usambazaji wa magonjwa ambukizi ukiwemo ugonjwa wa Ebola.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha (kulia) akizungumza na waandishi wa habari juu ya udhibiti wa magonjwa ya mlipuko kwenye kiwanja hicho. Hivi karibuni ugonjwa wa Ebola umetangazwa kutokea nchini Kongo.

Akizungumzia kuhusiana na mikakati hiyo ya kupambana na magonjwa ambukizi ukiwemo wa Ebola,  Afisa Afya Mfawidhi wa JNIA, Dkt. George Ndaki amesema wanatoa mafunzo kwa watumishi na wahusika wote wanaotumia kiwanja hicho katika kujikinga na magonjwa hayo.

Sisi tumejiandaa vizuri na tumeshafanya jitihada zote tumeshatoa maelekezo, mafunzo na kamati mbalimbali za kiwanja zimejipanga kudhibiti magonjwa yote ya kuambukiza, ikiwemo sisi wenyewe kujikinga na kuwakinga na abiria wote wanaotoka katika nchi hatarishi”, amesema Dkt. Ndaki.

Aidha akizungumzia kuhusiana na utaratibu ambao Kiwanja kimeweka ili kuhakikisha abiria wenye maambukizi wanapokelewa kwa tahadhari, ambapo wanapowasili na ndege zinazotoka nje ya nchi zinazopakia abiria wanaosafiri kutoka katika nchi zinazoshirikiana na Kongo hutakiwa kusafisha mikono kwa dawa maalum mara waingiapo katika eneo la kuwasili.

Pia abiria hao wanapoingia katika lango la kuwasili la abiria kutoka nje ya nchi, kumekuwa na mashine maalum inaangalia joto la mwili na likizidi nyuzi joto 38 wanamtaka kutoa maelezo Zaidi ya afya yake.

Abiria wote wanapowasili hupita katika eneo maalum ambalo wote hutakiwa kuosha mikono, lakini pia kuna mashine ambazo zimewekwa ili kuweza kuwatambua abiria ambao wanawasili wakiwa na hali ya joto isiyokuwa ya kawaida mfano kuwa na joto la juu sana kuanzia 38oC, ukiachana na hilo kuna fomu maalum ambazo abiria wanapowasili hujaza na pia taarifa kutoka kwa rubani wa ndege kama kuna abiria ana maambukizi kwenye ndege. Baada ya kumtambua mgonjwa basi atapitishwa katika njia ya tofauti na abiria wengine na kupakiwa katika gari la wagonjwa na kupelekwa Temeke Hospital,” amesema Dk. Ndaki.

Naye Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha akitoa ufafanuzi juu taarifa za uwepo wa ugonjwa wa Ebola, ameeleza kuwa tayari JNIA wanazo taarifa za mlipuko wa ugonjwa huo na taratibu zote zimeshachukuliwa kwa kuwakagua abiria wanaotoka nje ya nchi.

Ugonjwa wa Ebola unaosambazwa kwa virusi vya Ebola, husababisha homa kali inayoweza kuambatana na kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni, machoni na sehemu nyingine za wazi na unaenea kwa haraka. Hivi karibuni umetangazwa kutokea nchini Kongo na kusababisha vifo.