Waziri wa katiba na sheria nchini Tanzania Dkt Asha-Rose Migiro.
Afisa sheria wa tume ya kurekebisha sheria Bw. Geiasi Mwaipaja, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam ambapo amefafanua kuwa mapendekezo hayo yamekabidhiwa kwa ajili ya kujadiliwa na baraza la mawaziri, kabla ya kwenda kujadiliwa bungeni na kuwa sheria.
Taarifa za marekebisho ya sheria hiyo, zimekuja kufuatia mjadala mkali ulioibuka bungeni hivi karibuni, ambapo mbunge wa Mihambwe Bw. Felix Mkosamali amesema vitendo vya rushwa, uchache wake pamoja na utaalamu duni vimekuwa vikisababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wanaotafuta haki katika migogoro ya ardhi inayowakabili.
Kwa mujibu wa Mwaipaja, marekebisho hayo yanatokana na sheria ya mabaraza ya ardhi ya kijiji, wilaya na mikoa kuonekana kushindwa kutatua migogoro ya ardhi inayoyakabili maeneo mengi nchini hivi sasa.
Aidha Mwaipaja ameongeza kuwa pia tume hiyo inataka kutunga sheria itakayotoa ulinzi wa kutosha kwa wazee nchini, kwa kuwa hivi sasa hakuna sheria maalumu inayosimamia haki kwa kundi la wazee na watu wenye umri mkubwa.