Saturday , 28th Feb , 2015

Mbunge wa Mbinga Magharibi Mh. Kapteni John Komba amefariki Dunia leo saa 10 jioni katika Hosptali ya TMJ Mikocheni.

Marehemu Kapt John Komba

Kwa Mujibu wa mtoto wa Marehemu Bw. Jerry Komba amesema kifo cha marehemu baba yake kimetokana na ugonjwa wa kisukari ambapo amedai kuwa sukari ilishuka ghafla akiwa nyumbani kwake Mbezi Beach Dar es salaam.

"Ni kweli mzee amefariki dakika 50 zilizopita, alikuwa nyumbani amekaa lakini sukari ilishuka ghafla na baadaye kidogo alifariki" amesema Jerry Komba mtoto wa marehemu alipozungumza na EATV leo saa 11:20 jioni..

Katibu wa mbunge huyo Bwana Gasper Tumaini amesema kuwa mbunge huyo alikimbizwa katika hospitali ya TMJ ambapo ndipo mauti yamemkuta.

Aidha Bwana Gaspaer Tumaini ameongeza kuwa mwili wa marehemu umehamishiwa katika hosptali ya Lugalo jijini Dar es salaam ambapo ratiba ya Mazishi bado haijafahamika.

Eatv imewatafuta Afisa habari wa Ofisi ya Bunge ndugu Owen Mwandumbya, Mkurugenzi wa Mambo ya nje na Elimu kwa umma bwana Jesse Mwakasyuka na katibu wa Bunge Dkt Thomas Kashilila bila mafanikio kwa kuwa hawakupokea simu.

Katibu wa itikadi na uenezi Nape Nnauye amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kwamba mwili umeondolewa TMJ Hospitali na kupelekwa kuhifadhiwa hospitali ya Jeshi Lugalo.

Kufuatia msiba huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Kapteni John Damian Komba, Mbunge, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa ya CCM na msanii hodari sana wa kizazi chake.

Katika salamu zake za rambirambi kwa Spika wa Bunge, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda na Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Abdulrahman Kinana, Mheshimiwa Kikwete amesema:

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Kapteni John Komba, ambacho nimejulishwa kuwa kimetokea mchana wa leo, Jumamosi, Februari 28, 2015, kwenye Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam.”

“Kwa hakika, sina maneno ya kutosha kuelezea kwa fasaha hasara ambayo taifa letu na chama chetu kimepata kutokana na kifo cha Kapteni Komba. Taifa letu limepoteza hazina kubwa na mtu muhimu.

Nimemjua Kepteni Komba kwa muda mrefu sana, nimefanya naye kazi, Alikuwa msanii ambaye kiwango chake cha usanii kilikuwa hakipimiki, alikuwa na sifa kubwa za uongozi, alikuwa mpenzi, mzalendo na mtu mwaminifu sana kwa taifa lake na katika jambo lolote aliloliamini.,” amesema Rais Kikwete katika salamu hizo.