Waziri wa viwanda na biashara Dkt Abdallah Kigoda.
Naibu msajili mkuu wa BRELA Bw. Hakiel Mgonja, ameiambia East Africa Radio kuwa matapeli hao hujifanya mawakala na watumishi wa wakala hiyo ambapo wakiwa katika majengo zilipo ofisi hizo, huchukua fedha kutoka kwa wananchi kwa ahadi hewa ya kuwahudumia.
Aidha, Mgonja amewataka wananchi kuwa makini dhidi ya matapeli hao wakati ambapo wakala hiyo inafanya jitihada za kuongeza ofisi zake hususani maeneo ya mikoani ili kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi.
Mgonja ameongeza kuwa ili biashara zijulikane kitaifa na kimataifa, kuna haja ya wananchi kwenda BRELA ili waelekezwe namna ya kuanzisha pamona na kusajili majina na biashara zao kwa lengo la kuziwezesha biashara husika kutambulika ndani na nje ya nchi.
Aidha, naibu msajili huyo wa BRELA amefafanua kuwa wakati wakala hiyo ikielekeza nguvu katika kufungua ofisi zake mikoani, wananchi wanaweza kupata huduma zake ambazo hivi sasa zinatolewa kwa njia ya mtandao, huduma ambazo ninahusiha upatikanaji wa fomu na kutafuta majina ya biashara kwa lengo la kutonakili majina ya biashara nyingine.