Wednesday , 31st Oct , 2018

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda, amewataka Shirika la Haki za Binadamu na mataifa mengine kutoingilia kampeni yake ya kutokomeza mashoga mkoa wa Dar es salaam, kwani vitendo hivyo havifai kwa jamii.

Akizungumza mapema leo na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Paul Makonda amesema kwamba kitendo hicho ni kinyume na sheria za nchi, na kwamba mashirika hayo ni lazima yaheshimu sheria na maamuzi binafsi ya nchi, kwa ajili ya faida ya vizazi vijavyo.

Akiendelea kuelezea suala hilo Paul Makonda amesema sheria za nchi zimeweka wazi kuwa vitendo hivyo ni kinyume na sheria za nchi, na iwapo wanaona ni sahihi kuruhusu ushoga, basi wawachukue na kwenda kuishi kwenye nchi zao.

“Ndugu zangu wa Haki za Binadamu nafahamu hili jambo nilishawahi kuligusa kipindi cha nyuma, na mataifa mengine ambao mataifa yao yamepokea na kukubali ushoga, sisi tunautamaduni wetu, tuna sheria zetu, msituingilie, kama nyinyi mnaona mashoga ni haki, wachukueni mkakae nao kwenye nchi zenu, lakini kwenye mkoa wetu hatuhitaji mashoga, hakuna haki ya mashoga, kwa sababu sheria imeweka bayana”, amesema Paul Makonda.

Hii leo Mkuu wa mkoa huyo amefanya mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia hatua anazozichukua ili kukomesha vitendo vya ushoga na biashara ya ngono jijini dar es salaam, ambapo ameamua kuunda kamati maalum ya kufuatilia watu wanaojihusisha na masuala hayo.