Naibu waziri wa maji, Amos Makala ameziagiza mamlaka za maji kwenye mikoa yote nchini kujenga na kuboresha mifumo ya maji taka ambayo itakusanya maji yote machafu yanayotumika majumbani, viwandani na kwenye taasisi mbalimbali ili kuweka mazingira safi na kuepusha magonjwa ya milipuko.
Naibu waziri wa maji, Amos Makala ambaye amewasili jijini Mbeya na kutembelea vyanzo vya maji vinavyomilikiwa na mamlaka ya maji mkoa wa Mbeya na kisha kukagua miundombinu ya maji safi na maji taka ya jiji la Mbeya, amesema amerizishwa na kazi ambayo inafanywa na mamlaka hiyo kisha akaziagiza mamlaka za maji kwenye mikoa mingine nchini kuhakikisha pia inajenga na kuimarisha miundombinu ya maji taka.
Akimtembeza na kumwonesha vyanzo hivyo vya maji, kaimu mkurugenzi wa mamlaka ya maji mkoa wa Mbeya, mhandisi Martin Kimambo amesema kwa sasa mamlaka hiyo inazalisha maji ya kutosha yatakayokidhi mahitaji ya jiji la Mbeya hadi mwaka 2017.
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya maji mkoa wa Mbeya, Jaji Atuganile Ngwala amemfahamisha naibu waziri kuwa mamlaka ya maji mkoa wa Mbeya kiutendaji imeshika nafasi ya tatu kitaifa kwa kuzalisha na kuondoa maji taka.