Sunday , 27th Mar , 2016

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ameonya makanisa yaliyomo katika mkoa huo kuacha migogoro na vurugu na badala yake kuendesha shughuli zake kwa amani na kwa kuzingatia sheria za nchi.

Makonda ameyasema hayo leo katika ibada ya Pasaka iliyofanyika kitaifa katika kanisa la Anglikana Mtakatifu Albano Upanga jijini Dar salaam.

Akiwa ameambatana na mke wake katika ibada hiyo, mara baada ya kutakiwa kutoa salam kwa waumini, Makonda amesema kuwa katika siku za hivi karibuni, vurugu, mapigano na mambo yasiyompendeza Mungu yamehamia makanisani kiasi cha kuhitaji ulinzi wa polisi wakati wa matukio mbalimbali yanayofanywa makanisani.

Amesema kuanzia sasa muumini yeyote atakayeomba ulinzi wa polisi kanisani, atakamatwa na kuwekwa ndani kabla mambo mengine hayajafuata

“Juzi kuna mama mmoja Kimara, ni kiongozi wa kanisa, anasema kuna shughuli kanisani, anaomba ulinzi, nikamuuliza wa nini, akasema unajua huku kuna rushwa…. Nikashangaa kusikia eti kanisani napo kuna rushwa!! Hadi leo siamini…. Sasa nasema yeyote atakaye piga simu kuomba ulinzi wa polisi kanisani namuweka ndani yeye mwenyewe”

Makonda amelitaka kanisa kumsaidia kutimiza wajibu wake kwa kunyoosha mienendo ya waumini wake huku akitumia nafasi hiyo kusisitiza agizo lake la kuwataka wakazi wa mkoa wa Dar es salaam kuhakiki silaha zao ndani ya siku 90.

“Kuanzia Julai 01, mwaka huu mimi mwenyewe nitaongoza msako wa kukagua silaha ambazo hazijahakikiwa, sitakuwa na huruma, wala sitamuangalia mtu usoni” Amesema Makonda.

Makonda amesema kuwa kwa sasa jiji la Dar es salaam haliko salama kutokana uwepo wa silaha ambazo hazieleweki.

Amewaomba waumini wa Kikristo ambao leo wanaadhimisha sikukuu ya Pasaka kujitolea kuchangia maendeleo ya mkoa ikiwa ni pamoja na kumaliza tatizo la madawati.