Saturday , 2nd Jul , 2016

Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kuwa na uvumilivu dhidi ya hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano katika ukusanyaji wa kodi na hatua dhidi ya viongozi wabadhirifu.

Mhe. Samia amesema hayo hii leo jijini Dar es Salaam, alipotembelea maonyesho ya biashara ya kimataifa ya sabasaba na kuongeza kuwa hatua hizo zinalenga kukuza uchumi wa watu na kurudisha heshima na nidhamu serikalini.

Katika hatua nyingine mama Samia amelitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutotoa viwango vya ubora kwa makampuni ambayo hayatatumia nembo ya Tanzania lengo la kufanya hivyo ni kutaka kuzitambulisha bidhaa za Tanzania katika mataifa mbalimbali.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Charles Mwijage, amesema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kukuza uchumi ambao kwa kiasi kikubwa utategemea uwepo wa viwanda hivyo kuwa na nembo ya bidhaa za Tanzania ni hatua moja wapo.