Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia
Mbatia amesema kuwa kikao cha halmashauri kuu ya chama hicho kilijibadilisha na kuwa kamati ya nidhamu ya chama hicho na kukubaliana kwa kupiga kura kumvua uanachama baada ya kumkuta na makosa ya kujihusisha na migogoro ndani ya cha hicho, kukashifu viongozi wa chama hicho na kutoa na kupokea rushwa ambapo makosa hayo yote aliyatenda wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu hatua zilizofikiwa na uongozi wa chama hicho kuhusu ukosefu huo wa nidhamu, na kuwataka wanachama wote wa chama hicho kuzingatia sheria na misimamo ya chama hicho inavyoelekeza.
Wakati huohuo Mbatia amesema ili kuhakikisha jitihada za Rais Magufuli na nia njema ya kupambana na mafisadi papa zinafanikiwa, aangazie na wale wote waliopora mali za watanzania kiujanjaujanja zikiwemo nyumba za serikali, mashirika ya umma, viwanda pamoja na ardhi.
Kuhusu uchumi, chama hicho kimebaini athari za kiuchumi zitokanazo na maamuzi ya viongozi kufuatia matamko mbalimbali ya serikali kuwa mizigo bandarini inapungua kila siku wakati watumiaji wa bandari zetu wakihamia bandari nyinginezo za nchi jirani.
Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho imeitaka serikali kuweka mipango endelevu kabla ya kutoa matamko yanayokinzana hasa kwa maswala ya elimu ya taifa ambayo ndiyo tegemeo la maisha kwa watanzania walio wengi.




