Wednesday , 9th Dec , 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli, leo ameshiriki zoezi la usafi katika kuadhimisha miaka 54 ya uhuru wa Tanzania bara.

Akiwa katika eneo la Feri jijini Dar es salaam ambako ndiko alipofanya usafi huo, Rais Magufuli amesema atashangazwa iwapo watanzania watasubiri siku moja nyingine ya kufanya usafi, na kutaka zoezi hilo kuwa endelevu kwa nchi nzima.

“Nitashangaa sana kwa mwaka mzima tunasubiri siku moja ili tufanye usafi, ni aibu Tanzania kuwa na kipindu pindu wakati mambo mengine yangewezekana, tuendelee kufanya usafi kwenye mazingira yetu ili kujiepusgha na magonjwa mbali mbali”, alisema Rais Magufuli.

Pia akiwa katika eneo la Feri Rais Magufuli alipata fursa ya kuzungumza na wavuvi ambao amewashukuru kwa kujitokeza na kusaidia katika zoezi hilo la usafi, na kuwaahidi kutatua matatizo yao waliyomlalamikia.

Rais Magufuli amewaahidi wavuvi hao kuwasaidia kupata mikopo ya kuendeleza shughuli zao za uvuvi ikiwa watajiunga katika ushirika na kuwa na viongozi wao.

Aidha, Dkt. Magufuli amewataka Wavuvi hao waweze kujiunga katika vikundi vidogo vidogo ili waweze kupata misaada kutoka serikali huku akiwaahidi kuyashughulikia matatizo yao haraka iwezekanavyo.

“Shida wanazozipata ukweli shida zao ni za msingi na katika kuzingatia suala la ujirani mwema hizi shida zao nitazishughulikia, inaonesha wanasumbuliwa na vikodi vidogo vidogo, wanasumbuliwa na vitu vingine ambavyo havina maana”, alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameongeza kuwa ameyachukuliwa matatizo ya wavuvi hao kwa uzito mkubwa na kwamba hatawaangusha huku akitaka wachague viongozi watakaoweza kutetea maslahi ya wanyonge.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amewataka wananchi wafanye zoezi hilo kuwa endelevu na sio kusubiri kufanyika mara moja kwa mwaka kwa kuwa usafi ndiyo utakaowaondolea magonjwa ya mlipuko yasiyo ya lazima.