Tuesday , 5th Jul , 2016

Wakazi katika mji mdogo wa Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe jana(Julai 4) walionesha kutokubaliana na madiwani wao baada ya kujitokeza kwa wingi kwenye Mbio za mwenge wakati viongozi wao hao wakisusia mbio hizo.

Kati ya madiwani 14 wa halmashauri ya mji wa Tunduma,ni diwani mmoja pekee France Sikanyika wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kutoka kata ya Chiwezi ndiye aliyejitokeza huku wenzie 13 wa Chadema wakiingia mitini kushiriki mbio za Mwenge.

Wakati viongozi hao wakionesha hali hiyo, mambo yalikuwa tofauti kwa wananchi kwani kila kona ambayo Mwenge ulipita waliulaki kwa wingi na kwa shangwe na nderemo.

Alipohojiwa na waandishi wa habari juu ya kutoshiriki kwa madiwani wa Chadema, mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Tunduma Erick Mapunda amesema hajui sababu, bali kama ilivyokuwa kwa mwenzao wa CCM nao walishirikishwa kwa kupewa taarifa.

Mapunda amesema anaweza kuzungumzia kitendo hicho baadaye iwapo madiwani hao watawasilisha kwake taarifa ya sababu iliyowafanya wasishiriki mbio za Mwenge kwenye halmashauri yao.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wetu katika eneo la Mkesha wa Mwenge,walilaani kitendo kilichofanywa na madiwani wao wakisema kinaonesha kukosekana kwa uzalendo wa kudumisha na kuimarisha tunu za Taifa.