Tuesday , 14th Apr , 2015

Wakazi wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wamelilalamikia Shirika la Umeme nchini TANESCO kutokana na kuwepo kwa watu matapeli wanaowaunganishia umeme katika maeneo yao.

Hayo yamesemwa na baadhi ya wakazi wa wilaya ya Lushoto wakati wakitoa malalamiko yao katika vyombo vya habari na kusema kuwa yupo kishoka ambae anajitambulisha kama mfanyakazi wa TANESCO na kufanya huduma za kuwawekea nguzo za umeme pamoja kuwaunganishia umeme majumbani mwao hivyo kuwataka wahusika wa TANESCO wawe na vitambulisho maalum ili iwe rahisi kwa wananchi kuwafahamu.

Kwa upande wake Daudi Hassani Mgaza ambaye ni Kaimu Meneja wa TANESCO wilaya ya Lushoto amesema wamebaini kuwa kuna ujenzi wa line feki ya kuwaunganishia wananchi umeme wakati wakiendelea na operesheni ya ukaguzi wa ujenzi wa line za umeme.

Mgaza ameongeza kuwa wataing'oa line hiyo sambamba na kuwataka wakazi wa maeneo mbalimbali wanapohitaji huduma hiyo kufika katika ofisi za TANESCO ili kupewa risiti zilizo halali na si kuungana na watu wasio rasmi.