Tuesday , 8th Jul , 2014

Ofisi ya taifa ya takwimu nchini Tanzania leo imetoa taarifa ya kiwango cha mfumuko wa bei kwa kipindi cha mwezi Juni mwaka huu huku ikionesha kuwa mfumuko wa bei umeanza kushuka.

Mkurugenzi wa sensa na takwimu za kijamii wa ofisi ya taifa ya takwimu Bw. Ephraim Kwesigabo.

Mkurugenzi wa Sensa na takwimu za kijamii Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa katika kipindi hicho, mfumuko umeshuka kutoka asilimia 6.5 mwezi Mei hadi asilimia 6.4, huku thamani ya manunuzi ya shilingi ya Tanzania nayo ikipanda na kuimarika kutoka wastani wa shilingi 66.72 mwezi Mei hadi asilimia 67.12.

Aidha, Bw. Kwesigabo amesema kwa ujumla kiwango cha mfumuko wa bei nchini hakitofautiani na kile cha nchi nyingine za Afrika Mashariki na kwamba kushuka kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kushuka kwa bei za bidhaa za vyakula ambazo ndizo huchukua sehemu kubwa ya matumizi.

Bw. Kwesigabo amesema kulingana kwa mfumuko wa bei kunaweza kuchangiwa na muingiliano wa manunuzi baina ya wakazi wa nchi za Afrika Mashariki.