Monday , 9th May , 2016

Takwimu za ugonjwa wa Kipindupindu zinaonyesha kuwa hadi kufikia jana, nchini jumla ya wagonjwa 21,262 waliougua ugonjwa huo tangu kutokea kwa mlipuko wake, na kati ya hao, watu 333 wamepoteza maisha hadi sasa.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu.

Taarifa iliyotolewa leo na Wizara ya Afya kwa Vyombo vya habari inasema kuwa takwimu za wiki iliyopita kuanzia tarehe 2 hadi 8 Mei 2016 zinaonyesha kuwa, kasi ya ugonjwa wa kipindupindu imeongezeka, ambapo idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa ni 138 na vifo 2, ikilinganishwa na wagonjwa wapya 104 walioripotiwa wiki iliyotangulia, sawa na ongezeko la asilimia 32.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Mikoa ambayo imeendelea kuongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wiki hii ni Kilimanjaro (58, kifo 1), Dar es Salaam (29) na Morogoro (22, kifo 1), Pwani (16) na Mara (15).

Katika wiki iliyopita, mikoa ambayo haikuwa na wagonjwa wa kipindupindu ni Kigoma, Dodoma, Mwanza, Geita, Singida, Shinyanga, Arusha, Tanga, Tabora, Lindi, Kagera, Rukwa, Katavi, Mbeya, Simiyu na Mtwara.

Aidha, Serikali imetoa onyo kwa wananchi wanaokaa kandokando ya Mto Pangani hususani mikoa ya Tanga na Kilimanjaro, kuwa maji ya mto huo si salama, kwa kuwa yamechafuliwa na vimelea vya kipindupindu.

Kutokana na Takwimu kuonyesha kuwa ugonjwa huo umeongezeka serikali imewataka wananchi wote nchini kuchukua tahadhari kubwa, hususan wakati wa huu wa mvua, ambapo kuna uwezekano mkubwa wa maji ya mvua kusambaza vimelea vya ugonjwa huu.

Aidha, wananchi wanashauriwa kutumia maji safi na salama na hii ni pamoja na kuhakikisha maji ya kunywa yanachemshwa au kutibiwa kwa dawa kama maagizo ya wataalam yanavyoelekeza.