
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameitangaza kesho siku ya Alhamisi, Novemba 5, mwaka huu, 2015, kuwa Sikukuu na siku ya mapumziko.
Rais Kikwete amefanya uamuzi huo, ili kuwawezesha Watanzania kushiriki katika sherehe za kuhitimisha Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne na kuingizwa madarakani Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zitakazofanyika katika viwanja vya Uhuru jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam leo Jumatano, Novemba 4, 2015 na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Yohana Sefue, Rais Kikwete ametoa uamuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyo nayo chini ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa.
Sherehe hizo zinarajia kuanza kesho saa 12 asubuhi ambapo wananchi wataruhusiwa kuingia viwanjani hapo, na zitahdhuriwa na Rais wa nchi tofautitofauti wa Afrika, wageni wengine mashuhuri akiwemo Mhubiri wa Kimataifa kutoka Nigeria TB Joshua ambaye ameshawasili nchini hapo jana.