Wednesday , 31st Oct , 2018

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawasaka katibu mwenezi wa CCM kata ya Mkolani, Zephilin Michael (43) na Katibu mwenezi wa chama hicho kata ya Buhongwa wilaya ya Nyamagana, Hasan Bushangama (43) kwa tuhuma za kubaka na kulawiti.

Nembo ya Chama cha Mapinduzi.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Oktoba 31, na Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna amesema Michael anatuhumiwa kumlawiti kijana anayekadiriwa kuwa na miaka 16 tukio lililotokea Oktoba 26, 2018 saa 11:30 jioni katika nyumba moja ya kulala wageni iliyopo kwenye kata hiyo.

Taarifa hiyo imesema mtuhumiwa alimuajiri kijana huyo kuuza kahawa mtaani kisha alimpangishia chumba katika nyumba hiyo ya kulala wageni ili pindi anapotoka kuuza kahawa awe anafikia hapo.

"Siku hiyo mtuhumiwa alifika kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni na kumuuliza mhudumu kama kijana wake yumo ndani ya chumba chake na akaelezwa kuwa yumo, alimfuata humo chumbani huku mhudumu akiendelea na shughuli zake,” amesema.

Amesema baada ya muda mfupi ilisikika sauti ya mtu akipiga kelele kutoka ndani ya chumba hicho na baadaye watu walipochungulia kupitia dirishani walimuona mtuhumiwa akimlawiti kijana huyo.