Friday , 23rd May , 2014

Jamii imetakiwa itambue umuhimu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupitia huduma ya katalogi ya ki-electroniki katika maktaba ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu katika vitabu.

Makamu wa Rais Dkt Mohammed Gharib Bilal, akipata ufafanuzi wa namna shughuli za maktaba zinavyoendeshwa nchini kutoka kwa mkurugenzi wa bodi ya huduma za Maktaba Dkt Ally Mcharazo. Katikati ni naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi. Jennister Mhagama.

Hayo yamesemwa na afisa bodi ya huduma za Maktaba Tanzania Comfort Temba alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa habari na maelezo Dar es Salaam, na kuongeza kuwa bado lipo tatizo la wananchi na wanataaluma kwa ujumla kutofahamu umuhimu wa matumizi ya TEHAMA katika utafutaji wa taarifa muhimu

Pia ametaja kuwa moja ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na bodi hiyo ni kuongezeka kwa wataalam wa ukutubi, kupitia chuo cha Bagamoyo kilichopo chini ya bodi hiyo ambapo kwa sasa kuna jumla ya wanafunzi 1093, na kueleza kwa sasa vituo 43 vya makitaba vimeongezeka katika ngazi za Tarafa, Wilaya na Mikoa.