Tuesday , 5th Jan , 2016

Kauli mbiu ya ''Hapa Kazi tuu'' imeanza kugeuka shubiri kwa baadhi ya watendaji ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea,urasimu mkubwa na bila kujali viapo vyao vya kazi .

Naibu waziri wa Ofisi ya Rais,Tamisemi,Utumishi na Utawala bora,Suleiman Jafo (MB) amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela John Wanga kutokana na matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

Jafo amefikia uamuzi huo baada ya kugundua kuwa Mkurugenzi huyo amekataa kuhamia kwenye nyumba ambayo hadi sasa inakadiriwa kugharimu milioni 200 na kukaa kwenye nyumba ya kupanga ambayo serikali inalipa milioni 2 kila mwezi jambo ambalo amevuka kiwango cha serikali cha shilingi laki nne.

Naibu waziri huyo ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa manispaa ya Ilemela na kusema kuwa Mkurugenzi huyo amekwisha ambiwa ahamie kwenye nyumba hiyo mpya jambo ambalo amekaidi hadi sasa.

Hata hivyo imebainika kuwa nyumba hiyo ilianza kujengwa toka 2013 na ilipokamilika Mkurugenzi huyo alikataa kwenda kukaa huko kutokana na kwamba haina kiwango na ipo sehemu hatarishi ukilinganisha na wadhifa wake.

Aidha Jafo amewakumbusha watendaji hao kuwaonea huruma wananchi ambao wanakwenda hopspitalini na kukuta dawa hakuna pia wawakumbuke kina mama wanaojifungulia chini kwa kukosa huduma wakati wao wanakataa kukaa kwenye nyumba kwa madai yasiyo ya msingi na kuzidi kuliingizia taifa hasara.