Wednesday , 29th Apr , 2015

Serikali ya halmashauri ya wilaya ya Iringa imesema kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa na tatizo la njaa kuanzia mwezi wa nane mwaka huu hadi kufikia mwezi wa pili mwaka kesho.

Ramani ya Mkoa wa Iringa.

Kaimu afisa kilimo umwagiliaji na ushirika Wilaya ya Iringa Silvester Muhoka amesema kuwa hali hiyo imechangiwa na tatizo la ukame na tarafa ya Ismani ndio itakayo athirika zaidi.

Amesema kuwa katika tarafa ya Pawaga hawana mashaka kuhusu janga hilo kutokana na kuwa halimashauri imeshaboresha miundombinu ya umwagiliaji.

Aidha amesema kuwa hali hiyo ya ukame inasababishwa na upungufu wa mvua kutokana na hali ya tabia nchi na kwa mwaka huu hali ya ukame imeonekana kuwa kubwa zaidi kuliko miaka iliyopita.

Hata hivyo ameongeza kwa kuwashauri wananchi waweze kulima mazao yanayoweza kustahimili ukame kama vile mtama, ulezi na mihogo ili kuepusha hali kama hiyo kujitokeza.