Monday , 24th Aug , 2015

Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Ludewa mkoani Njombe, Deo Filikunjombe ametangazwa kuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo bila kupingwa

Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Ludewa mkoani Njombe, Deo Filikunjombe ametangazwa kuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo bila kupingwa baada ya mgombea ubunge wa CHADEMA Bwana Batholomeo Mkinga kukosa sifa za kugombea nafasi hiyo kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya ujazaji wa fomu.

Shangwe za baadhi ya wananchi na wanachama wa chama cha mapinduzi wilaya ya Ludewa zimeshuhudiwa, wakifurahia mbunge wao, Deo Filikunjombe kutangazwa kuwa mgombea pekee wa Ludewa baada kupita bila kupingwa katika kinyang'anyiro hicho kutokana na mgombea wa CHADEMA kukosa sifa kwa kushindwa kujaza fomu namba 10 ya tamko la mgombea.

Miongoni mwa wagombea kupitia chama cha Tanzania Labour Party (TLP) bwana Blanka Haule aliyeshindwa kabisa kurejesha fomu, anasema wana-Ludewa wanahitaji maendeleo na kwamba Filikunjombe anatosha.

Pamoj na baadhi ya vijana wa Ludewa wakiwemo waendesha boda boda kujianzishia tafrija fupi ya kuzunguka mji wa Ludewa na kuonesha michezo yao ya pikipiki wakiashiria furaha, baadhi ya wanachama wa CCM waliomsindikiza mbunge wao kuchukua barua ya uthibitisho wa kuwa mgombea pekee katika jimbo hilo wametoa yao ya moyoni na kusema wanamuhitaji Deo Filikunjombe.

Lakini Deo Filikunjombe mwenyewe amewashukuru wananchi wake na kusema huo ni ushindi wake na wana-Ludewa kwa ujumla.