Friday , 7th Nov , 2014

Tume ya ushindani nchini FCC imeshateketeza bidhaa bandia zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tano tangu ilipoanza kufanya kazi ambapo baadhi ya watuhimiwa waliokuwa wanajihusisha na uingizaji na uuzaji wa bidhaa bandia wakipewa adhabu kali

Baadhi ya bidhaa bandia zilizowahi kukamatwa na tume ya ushindani nchini Tanzania

Akiongea kwenye mafunzo ya wadau wa masuala ya biashara wakiwemo viongozi wa serikali, sekta binafsi, wazalishaji na watumiaji wa bidhaa mbalimbali mkoani geita Mkurugenzi wa utafiti kutoka tume ya ushindani nchini FCC, Alaan Mlula amesema utendaji kazi wa tume hiyo pia umesaidia kupunguza uingizaji na matumizi ya bidhaa bandia na kuimarisha mfumo wa uchumi na ushindani, kumlinda mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia.

Mkurugenzi huyo ameshauri wadau kupiga vita matumizi ya bidhaa hizo badala ya kusubiri tume kupambana na kuziteketeza katika soko kwani mchakato huo una gharama kubwa na unahitaji rasilimali nyingi wakiwemo wataalam na fedha:..

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Manzie Mangochie ameshauri wananchi kufahamu kwamba suala la bidhaa bandia ni tatizo kubwa linalohitaji nguvu ya pamoja kukabiliana nalo kwani matumizi ya bidhaa hizo yameshaleta madhara makubwa kijamii na kiuchumi na hivyo ametoa wito kwa wadau kuendelea kuelimishana.