Monday , 15th Aug , 2016

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, amewaongoza mamia ya wananchi wa Zanzibar katika maziko ya Rais wa Pili wa Serikali hiyo, Aboud Jumbe Mwinyi aliyefariki dunia jana nyumbani kwake jijini Dar es salaam.

Shughuli ya maziko ya Marehemu Aboud Jumbe iliyofanyika leo mchana visiwani Unguja

Maziko hayo yamefanyika katika Makaburi ya Migombani Unguja, na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa wa serikali, wakiwemo wastaafu katika ngazi mbalimbali.

Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape nnauye, Rais Mstaafu wa awamu ya pili wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ally Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, Mbunge wa Chalinze Ridhiwan Kikwete, Rais Mstaafu wa Zanzibar Aman Abeid Karume, Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar Maalim Seif Hamad, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na wengine wengi.

Akimuelezea marehemu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan amemwelezea hayati Aboud Jumbe Mwinyi kama kiongozi ambaye aliitetea demokrasia pamoja na kufanya kazi kwa wazanzibari kwa kuimarisha umoja na mshikamano.

"Marehemu Aboud Jumbe ni baba wa demokrasia kwa Zanzibar yeye ndiye alirejesha mfumo wa kupiga kura, akaanzisha Baraza la Wawakilishi pia ndiye aliyendeleza mfumo wa ujenzi wa nyumba vijijini hivyo ni kiongozi ambaye hawezi kusahaulika kwa mchango wake katika maendeleo ya wazazibar''- Amesema Mama Samia.

Aidha kwa upande wake Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi Bin Ally amesema busara na hekima ambayo ameioneshs katika kipindi cha uongozi wake na hata baada ya kuachia uongozi ni jambo linalopaswa kutiliwa maanani katika kujenga nchi yenye amani na mshikamano.

Wakati huo huo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Prof. Benson Bana amesema katika historia ya ukombozi wa Zanzibar Marehemu Jumbe hawezi kusahaulika kwa mchango wake mkubwa kwa kisiwa hicho na Tanzania bara katika kudumisha Muungano.

Hayati Aboud Jumbe Mwinyi alifariki dunia Jumapili ya tarehe 14. Agosti 2016 akiwa na umri wa miaka 96 ambapo ameacha watoto 13 na wajukuu 40.
Akisoma  risala wakati wa shughuli ya maziko ya Kiongozi huyo mashuhuri Tanzania Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais  Mohammed Aboud Mohmamed amesema Marehemu alisoma skuli ya bembela mnamo mwaka 1930 hadi 1942.

Akaendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Ugandakatika ngazi ya diploma ya ualimu na baada ya hapo akahudumu kama mwalimu katika shule ya Lumumba kuanzia mwaka 1946 hadi 1952.

Hayati Jumbe alishika nafasi ya Urais wa Zanzibar baada ya kifo cha hayati Abeid Amani Karume kuanzia April 7 waka 1972 na kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Zanzibar hadi mwaka 1984.

Baadhi ya mambo ambayo atakumbukwa nayo sana ni pamoja na kuendeleza makazi ya vijijini Kisiwani Zanzibar, kuendeleza mfumo wa kupiga kura, pamoja na kuanzisha Baraza la Wawakilishi.

Hayati Jumbe alifariki dunia Agosti 14 mchana nyumbani kwake Kigamboni Mji Mwema Jijini Dar es salaam na kuzikwa kisiwani Zanzibar ambapo alikataa kuzikwa kwa heshima za kupigiwa mizinga na kutaka azikwe kwa heshima za kiislamu jambo ambalo limezingatiwa.

Hayati Jumbe amefariki akiwa na umri wa miaka 96 na ameacha watoto 14 na wajukuu 40.

Sisi wote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea. Amen.

Aboud Jumbe Mwinyi enzi za uhai wake