Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amesema ofisi ya katibu wa bunge imewanyima watanzania fursa kujua hatma ya ripoti ya uchunguzi uliofanywa na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, TAKUKURU, kuhusu sakata la Escrow baada ya kutupilia mbali ombi lake la kutaka kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili kuitaka serikali iwasilishe bungeni ripoti hiyo kwa lengo la kuijadili na kutolewa maamuzi zaidi.
Kafulila amesema kuwa Januari 28 mwaka huu alimuandikia katibu wa bunge kuomba atoe hoja binafsi bungeni ili kuitaka serikali iwasilishe ripoti ya uchunguzi wa TAKUKURU kuhusu sakata la Escrow kwa madai kuwa ripoti hiyo ina mambo muhimu yanayopaswa kujulikana kwa watanzania, lakini ofisi ya katibu wa bunge imemjibu kwa barua kuwa suala hilo haliwezi kujadiliwa tena bungeni hatua ambayo amedai kuwa ni kuwanyima watanzania fursa ya kujua hatma ya suala hilo.
Akijibu maswali ya wandishi wa habari waliotaka kujua nini kifanyike ili suala hilo lifike mwisho na watanzania waanze kujadili mambo mengine, Kafulila anasema mambo matatu yanahitajika ambayo ni kuwafukuza kazi watuhumiwa, kuwafikisha mahakani na kurejesha fedha za umma walizochota.
Kuhusu minong’ono ya kwamba anatumika na baadhi ya watu na taasisi kushinikiza suala hilo, Kafulila anasema kuwa tuhuma hizo hazina ukweli wowote na kwamba zinatokana na kutapatapa kwa watuhumiwa wa sakata hilo kutaka kujisafisha.