Thursday , 17th Dec , 2015

Wananchi waliojenga na kuweka makazi ya kudumu katika eneo la Jangwani/Mkwajuni jijini Dr es salaam wamekumbwa na taharuki baada ya kazi ya kubomoa nyumba zao kuanza hii leo chini ya Manispaa ya Kinondoni

ikishirikiana na maafisa ardhi pamoja na uongozi wa baraza la kuhifadhi mazingira hapa nchini.

Wakizungumza kwa uchungu baada ya kukumbwa na bomoa bomoa hiyo wananchi hao wamesema wameshtushwa na zoezi hilo kuja ghafla bila wao kupewa taarifa za kufanyika kwa ubomoaji huo huku wakiwa hawana mahali pa kujihifadhi wao na mali zao.

Mmoja wa wananchi hao Bwn Hasani amesikika akisema kwamba wameishi katika eneo hilo kwa muda mrefu sana na wanalipia huduma zote za kijamii kama vile umeme,maji na wanapewa risiti hivyo imewashangaza mno kuona kwamba leo serikali inawaambia haiwafahamu.

'' Sisi tunashangaa sana kwa serikali kutufanyia hivi mimi nadhani hawa watendaji hawamuelewi Rais Dr. Magufuli anaposema hapa kazi tuu hamaanishi waje kutuumiza sisi wananchi tuliomchagua maana haiingii akilini kwamba hawa watu wa ardhi wanakuja kutupimia viwanja na tunawekewa umeme na maji na tunalipa kodi zote sasa hii ya kusema tupo kinyume na hatutambuliki inatoka wapi''. Alihoji Bwn. Hassani.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Baraza la hifadhi ya mazingira (NEMC) Bwn. Manchare Heche amesema kuwa watawabomolea wananchi wote ambao wamejenga katika eneo lote la bonde la mto msimbazi na lengo la serikali ni jema kwa kuwa wanataka kuwalinda wananchi ili wasipoteze maisha kutokana na mvua na vile vile eneo hilo si salama kwa makazi ya binadamu.

''Tutabomoa kwa wananchi wote ambao wapo katika eneo hili na sii hawa tuu wananchi wote waliojenga maeneo ya mabondeni na kando kando ya mito umbali wa mita 60 tutabomoa nyumba zao zote na hata kama wameweka maeneo ya kibiashara tutabomoa ili kulinda afya zao pia kulinda mazingira''. Amesisitiza Bwn.Heche.

Aidha Bwn. Heche amewakumbusha wananchi wa eneo hilo la jangwani kwamba Rais Mstaafu Dr. Jakaya Kikwete aliwagawia wananchi viwanja baada ya kukumbwa na mafuriko na wakapewa katika eneo la Mabwepande lakini wananchi hao wakarudi tena katika eneo la Jangwani na sasa serikali imeamua kuwabomolea nyumba zao na zoezi hilo litakua endelevu.