Thursday , 10th Jul , 2014

Waendesha bodaboda Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, leo wamehoji ipo wapi dhana ya wao kujiajiri, huku mamlaka ya mkoa na jiji hilo zikiwazuia kuingia na abiria kwenye maeneo ya katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Pikipiki za magurudumu mawili maarufu kama boda boda.

Akizungumza na East Africa Radio, Afisa Habari wa Jumuiya ya wendesha Bodaboda jijini Dar es Salaam Bw. Abdallah Bakari amemuomba rais Jakaya Kikwete kuingilia kati kwa kutengua amri ya wao kutoingia na abiria katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Aidha, Bakari pia amemuomba Rais Kikwete afanye uchunguzi kuona iwapo watendaji wakuu katika mkoa wa Dar es Salaam wanamsaidia katika kutekeleza ahadi ya chama tawala CCM iliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ya kwamba kuongeza ajira kwa vijana.

Mapema wiki hii, baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa baadhi ya askari wa doria ya pikipiki maarufu kama Tigo wamekuwa wakichukua rushwa kutoka kwa waendesha pikipiki kwa madai ya kutekeleza sheria ya kutoingia katikati ya mji.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini DCI Issaya Mngulu alisema kitendo hicho ni kinyume na maadili ya jeshi la polisi, huku akizungumzia haja ya kufanyika kwa mabadiliko ya usimamizi wa sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa faini za papo kwa papo kwa makosa ya barabarani.