Wednesday , 31st Oct , 2018

Kada wa Chama Cha Mapinduzi na Msanii wa zamani wa muziki wa Hiphop, Seleman Msindi (Afande Sele) amependekeza kuongezewa kwa ulinzi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kile alichokidai kuwa kiongozi huyo anafanya kazi ya hatari zaidi.

Kada wa CCM Seleman Msindi.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Afande sele ameandika “huu ndiyo ukweli kutoka ndani ya moyo wangu nasema hivi, kama mimi ningekua ni miongoni mwa wabunge wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania,bila shaka ningepeleka hoja binafsi ya kutaka Rais Magufuli aongezewe ulinzi mkubwa maradufu kama ule wa Rais Kim Jong Un wa North Korea,Donald Trump wa Marekani".

Aidha Afande sele ameendelea kwa kuandika “pia ningeomba hao walinzi wake walipwe mishahara na posho nyingine kwa kiwango cha upendeleo. huu ni mtazamo wangu na wala usijenge chuki kwakuwa na wewe unamtazamo wako na wala hatutavunja urafiki.”

Katika andiko hilo, Afande sele ameambatanisha na picha ambayo inamuonesha ndugu wa mfanyabiashara, Rostam Aziz bwana Iqram Aziz kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kukutwa na silaha za moto na meno ya tembo zikiwa nyumbani kwake bila kibali cha mkurugenzi wa wanyama pori Tanzania.

Afande Sele ni miongoni mwa waliokuwa makada wa Upinzani kupitia Chama Cha ACT-Wazalendo ambao walitamngaza kuhamia Chama Cha Mapinduzi wakati Rais Magufuli alipokuwa kwenye ziara mkoani Morogoro kwa nia ya kumuunga mkono Rais kwa kazi anayoifanya.