Jumanne , 19th Mei , 2015

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zacharia Hans Pope amesema, bado hawajajua ni kocha yupi ama mzawa au kutoka nje ya nchi atakayerithi mikoba ya kocha aliyeondoka katika kikosi hicho, Goran Kopunovic.

Akizungumza na East Africa Radio, Hanspope amesema, Goran aliondoka mara baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi kuu soka Tanzania Bara msimu huu uliomalizika baada ya kushindwa katika suala zima la malipo kwani kocha huyo alikuwa akihitaji kipato kikubwa ili aweze kusaini mkataba wa kuendelea kukinoa kikosi hicho hela ambazo Klabu hiyo hazina.

Hanspope amesema, hivi sasa Klabu hiyo inaendelea kutafuta kocha ambaye ataweza kuendana na mahitaji ya timu hiyo na kukinoa kikosi hicho katika michuano ya ligi kuu soka Tanzania Bara msimu ujao.

Hanspope amesema, katika suala zima la kumlipa kocha atakayepatikana hawatahitaji mfadhili atakayemlipa kocha bali watahitaji vyanzo vya mapato kutoka ndani ya klabu hiyo kwani masuala ya wafadhili huwa yanakwama pale mfadhili anapopata matatizo hivyo huleta matatizo katika kutimiza malipo kwa kocha huyo.