Katibu wa Muungano wa Vyama vya Madereva, Rashid Salehe, akizungumza na madereva akiwa ameambatana na Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo Bw. Shaban Mdemu.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi kutoka vyama vingine vya madereva, Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo Bw. Abdallah Lubala amesema kimsingi wamekubali kushiriki kwenye tume iliyoundwa na waziri mkuu ambayo jukumu lake litakuwa ni kushughulikia kero zote zinazohusu sekta ya usafirishaji nchini.
Kwa mujibu wa Lubala, kwa sasa umoja huo unashughulikia suala la uteuzi wa wajumbe watakaowakilisha umoja huo kwenye tume iliyoundwa na waziri mkuu na kwamba wao ndio watakaokuwa wawakilishi wa hoja zao kwenye mazungumzo hayo.
Aidha kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda ambaye ndiye aliyehusika kuwashawishi madereva kukubali wito wa kuwa sehemu ya tume hiyo, amesema hatua iliyofikiwa baina ya serikali na madereva itasaidia kumaliza kero zote zinazohusu sekta ya usafiri hasa madai ya madereva ya kuwepo kwa ajira za kudumu pamoja na mazingira bora ya kazi.
Makonda amewataka wanasiasa nchini kuacha kutumia migomo na matatizo mengine yanayotokea kwenye jamii kama mtaji wao wa kisiasa na kwamba badala ya kufanya hivyo, ni bora wakaungana kama taifa katika kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa moja siku zote.