Baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma kusema taarifa za ajali zinazosambaa kwenye mtandao wa kijamii wa TikTok zikimhusisha msanii wa muziki, Zuwena Mohamed maarufu Shilole kuhusu kunusurika katika ajali ya gari usiku wa kuamkia Januari 3, katika eneo la Malagarasi mkoani Kigoma hazijaripotiwa popote, msanii huyo ameandika ujumbe wa shukrani kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote waliomtumia salamu na kumuombea baada ya kunusurika katika ajali hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram @OfficialShilole, Shilole amesema amemwona Mungu kwa macho yake na kwamba baada ya ajali hiyo bado yuko hai kwa neema zake akiwashukuru wote waliomtumia jumbe, waliompigia simu yeye pamoja na watu wake wa karibu, na kumuombea, akieleza kuwa hakika Mungu ni mwema sana.
Awali, taarifa ya ajali ya Shilole ilitolewa Januari 3, 2025 wakati akitoka kwenye hafla ya Pilau Day iliyoandaliwa na mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus maarufu Baba Levo, akieleza kuwa msanii huyo alipata ajali eneo la Malagalasi mkoani Kigoma, umbali mfupi kabla ya kuingia Mkoa wa Tabora, akielekea jijini Dodoma.
Baba Levo alisema gari walilokuwa wakitumia liligonga ng’ombe aliyekuwa barabarani, na kwamba msanii huyo amepelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.


