
Mahakama Kuu Masjala Ndogo jijini Dar es Salaam imekubali pingamizi lililowasilishwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, na kukataa kupokea kielelezo cha flash na kadi ya kumbukumbu kama ushahidi.
Uamuzi huo umetolewa Jumatano, Oktoba 22, 2025, na Jaji Dustan Nduguru, ambaye anaongoza jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo.
Katika hoja zake, Lissu aliwasilisha sababu nne za kupinga upokelewaji wa vielelezo hivyo, akieleza kuwa shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, Inspekta wa Polisi Samwel Kaaya (39), hana ujuzi maalum katika uchambuzi wa video, bali ni mtaalamu wa picha tuli (still photography).
Mahakama imekubaliana na hoja hizo na kutoa uamuzi kwamba, shahidi huyo hana sifa zinazostahili kitaalamu kuwasilisha vielelezo vya video mbele ya mahakama.