Jumapili , 19th Oct , 2025

Mazishi rasmi yatafanyika leo Jumapili huko Bondo Kaunti ya Siaya nchini humo. 

Mwili wa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga ambao unatarajiwa kuzikwa leo huko kaunti ya Siaya umewasili katika safari yake ya mwisho katika ngome yake ya kisiasa ya Nyanza ukibebwa ndani ya ndege ya Jeshi la Wanahewa la Kenya Leonardo C-27J Spartan.

Odinga alifariki dunia Oktoba 15, 2025, akiwa na umri wa miaka 80, akiwa nchini India. Mapema baada ya kifo chake Kamati ya Kitaifa inayoratibu mazishi ya Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya, ilitangaza kuwa mazishi yake yatafanyika leo Jumapili nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya.

Hayo yanajiri wakati ambapo familia ya Odinga ikiomba mazishi yafanyike haraka ndani ya saa 72 mara baada ya baada ya kifo chake kama alivyoomba Odinga enzi za uhai wake.

Mnamo siku ya Ijumaa shughuli ya kuaga mwili wa Odinga iliendelea katika Uwanja wa Nyayo ambapo viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Kenya walishiriki.

Pia, maelfu ya waombolezaji kutoka jiji la Kisumu na maeneo mengine ya Magharibi mwa Kenya walijitokeza siku ya jana Jumamosi kumuaga aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, kiongozi mashuhuri, aliyetawala siasa za eneo hilo katika kipindi chote cha uhai wake.

Kisumu ndio ilikuwa ngome kuu ya kisiasa ya Odinga, jiji ambalo aliishi akiwa mtoto mdogo. Mazishi rasmi yatafanyika leo Jumapili huko Bondo Kaunti ya Siaya nchini humo.