
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wazi msimamo wake kuhusu hali ya kisiasa nchini, ikisisitiza kuwa hakuna sheria yoyote iliyovunjwa katika utekelezaji wa majukumu yake kama taifa huru linalozingatia utawala wa sheria.
Akizungumza na wahariri jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema kuwa serikali imekuwa wazi na ya uwazi kuhusu masuala yote yanayohusu mwenendo wa kisiasa nchini. “Hatujavunja sheria yoyote ile na tumeendelea kuzingatia sheria,” alisema Balozi Kombo.
Kauli hiyo imekuja kufuatia sintofahamu iliyojitokeza miongoni mwa baadhi ya wanasiasa wa upinzani, baada ya vyombo vya dola kumshikilia Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na shtaka la uhaini.
Lissu alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025.
Katika hatua nyingine, Waziri Kombo amewataka wanadiplomasia wanaowakilisha mataifa yao nchini kuheshimu masharti ya Mkataba wa Vienna.
Amesisitiza kuwa hairuhusiwi kwa wanadiplomasia kufika mahakamani bila kibali rasmi kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Nje, akieleza kuwa ni muhimu kufuata taratibu za kidiplomasia kama ilivyoainishwa katika mkataba huo wa kimataifa.
Aidha Serikali imeendelea kusisitiza kuwa itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, na kwamba haki na taratibu zote za kisheria zitafuatwa ipasavyo kwa kila mwananchi, bila kujali nafasi yake ya kisiasa na Kijamii.