Jumanne , 25th Feb , 2025

Mamia ya watu nchini Argentina wamehudhuria misa maalum kwa ajili ya kumuombea kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis, ambaye amelazwa hospitali akiwa katika hali mbaya huku taarifa zikieleza kuwa hali yake imeanza kuimarika kidogo

Watu hao walikusanyika katika mji alikozaliwa wa Buenos Aires wakati akiwa askofu mkuu kabla ya kupewa upapa, alipokuwa akiongoza misa na kupinga ukosefu wa usawa na dhulma.

Taarifa ya Vatican imesema hali ya kiafya ya kiongozi huyo wa kidini bado sio ya kuridhisha japo imeimarika kidogo. 

Taarifa hiyo inaeleza kuwa hali ya kiafya ya Baba Mtakatifu, ingawa ni mahututi, inaonyesha kuboreka kidogo.
Hata leo hakukuwa na dalili za matatizo ya kupumua kama pumu, baadhi ya vipimo vya maabara vimeonyesha kuboreka.

Papa Francis anapokea matibabu ya nimonia katika Hospitali ya Gemelli mjini Rome na leo ikiwa ni siku ya 12 tangu apelekwe hospitalini hapo na hali yake imeanza kuimarika tofauti na siku mbili zilizopita.

Jumapili jioni, Vatican ilitoa taarifa kuwa hali ya Papa Francis ilizidi kuzorota na aliwekwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu, huku akipumua kwa msaada wa mashine.

Vatican iliongeza matatizo madogo ya figo ya Papa, yaliyotangazwa mara ya kwanza Jumapili, hayatoi wasiwasi huku akiendelea kupatiwa tiba ya oksijeni.

Leo ni siku ya 11 kwa Papa Francis mwenye umri wa miaka 88, tangu alipolazwa hospitali, ikiwa ndio muda mrefu zaidi kukaa hospitali katika muda wa karibu miaka 12 aliyohudumu kama Papa.