Jumatatu , 24th Feb , 2025

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumatatu, Februari 24, 2025, amezindua jengo jipya la Halmashauri ya Bumbuli, mkoani Tanga, akisisitiza umuhimu wa miradi ya maendeleo kwa wananchi. 

jengo jipya la Halmashauri ya Bumbuli

Mara baada ya kuzindua jengo hilo, Rais Samia ameeleza furaha yake kwa kupokelewa vizuri na wananchi wa Bumbuli wakiongozwa na Mbunge wao January Makamba akisema amefurahi pia kuona mabango ya upendo kutoka kwa wananchi ambayo yanayosomeka: "Tunakupenda sana Mama."

Rais Samia amewashukuru wakandarasi, washauri, na wafanyakazi wa Halmashauri kwa juhudi zao katika kuhakikisha jengo linakamilika kwa ubora, akisema kuwa kazi yao ni mfano mzuri wa ushirikiano wa kiutendaji. 

Vilevile ameeleza kuwa, jengo hilo limejengwa kwa lengo la kuhakikisha watumishi wa Halmashauri wanafanya kazi katika mazingira bora na wananchi wanapata huduma kwa urahisi.

"Jengo hili ni la wananchi wa Bumbuli. Huduma zote zitapatikana hapa, na naomba mlitumie kwa manufaa yenu. Lengo letu ni kuboresha huduma kwa wananchi na kutoa fursa kwa watumishi wetu kufanya kazi zao kwa ufanisi," alisema Rais Samia.

Kwa uzinduzi huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekazia dhamira yake ya kuhakikisha maendeleo yanaendelea kusogea kwa kasi na wananchi wanapata huduma bora karibu.