Jumatano , 6th Nov , 2024

Binti wa miaka 13 ambaye amehitimu darasa la saba mwaka huu katika shule ya msingi Rulanda iliyoko wilaya ya Muleba mkoa wa Kagera, anadaiwa kubakwa na mwalimu wa taaluma katika shule hiyo aitwaye Lameck Jonas Bahikwaki ambaye inadaiwa ametoroka baada ya tukio hilo.

Mwanafunzi anayedaiwa kubakwa

Mtoto huyo ambaye jina lake limehifadhiwa ameeleza kuwa alifika shuleni hapo Oktoba 30 mwaka huu saa tisa alasiri kufuatilia matokeo yake ya mtihani wa taifa wa kuhitimu darasa la saba na kumkuta mwalimu huyo, ambaye alimweleza kuwa matokeo yake sio mazuri lakini aondoke arudi tena saa kumi ili aone namna ya kumsaidia. 

Amesema aliporudi shuleni saa 10:00 jioni aliingia katika darasa walilokuwa wakilitumia kusoma, na ghafla mwalimu huyo aliingia na kufunga mlango akamvua nguo kwa nguvu na kumpaka dawa sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwamo katika sehemu zake za siri, na nyingine akamnywesha na kusababisha azimie.
 
Wakazi wa kijiji Rulanda kata Rulanda lilipotokea tukio hilo wamesikitishwa na kulaani kitendo hicho na kuiomba serikali kuwasaidia kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa watoto ambavyo vimekithiri na kuwafanya kuishi kwa hofu.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Muleba Isaya Mbenje amekiri kupokea taarifa ya tuhuma za mwalimu huyo kumbaka mtoto na kuwa wanaendelea kuwasiliana na jeshi la polisi ili kuhakikisha anasakwa na kupatikana.