Alhamisi , 10th Oct , 2024

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amewataka viongozi wa CCM kutenda haki kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, Novemba mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi

Akizungumza na viongozi na wanachama mbalimbali wa CCM Wilaya ya Kahama leo, Oktoba 10, 2024, amesema kila mwanachama wa CCM ana haki sawa na mwingine, akisisitiza kuwa ni kinyume cha maadili ya CCM kumnyima mtu mwenye sifa bora nafasi ya uongozi kutokana na chuki binafsi.

"Tunakoelekea kwenye chaguzi zetu, utekelezaji wa haki unatakiwa acheni kupanga safu, viongozi bora ndio wapitishwe ni kosa kubwa la kimaadili ndani ya CCM kiongozi kumkamia mwanachama kwamba eti safari hii nitahakikisha fulani anakatwa kwenye chama chetu hiyo hapana, kwani kila mwanachama ndani ya CCM ana haki sawa na mwingine," amesema Balozi Dkt Nchimbi

Aidha ameongeza kuwa, "Tuna watu, ukimalizika tu uchaguzi ndani ya chama chetu, anaanza upelelezi nani ambaye hajamuunga mkono na kuanza kumshughulikia hiyo ni tabia mbaya na haikubaliki kwani mtu kukupigia kura ni haki yake, akikunyima kura ni haki yake pia kuna wengine viongozi wamejigeuza kuwa miungu watu hiyo hapana viongozi wazuri husambaza upendo,"amesema Balozi Nchimbi.

Katibu wa Idara ya Itikadi, Uenezi, na Mafunzo ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Amos Makalla, ametoa wito kwa Watanzania na wanachama wa CCM kujiandikisha katika daftari la makazi ili kuhakikisha wanapata fursa ya kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Aidha, Makalla amewataka mabalozi wa CCM kote nchini kushirikiana na wananchi kwa kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, akieleza kuwa hatua hiyo itawawezesha kuchagua viongozi bora kutoka ndani ya chama.