Wanakikundi cha kijamii
Wakiongea wakati wa ziara ya ujumbe kutoka Jamhuri ya Siera Leone waliofika Kata ya Lugarawa na kutembelea vikundi vinavyofanya kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara katika kata hiyo wanakikundi hao wamesema tangu waingie mikataba na TARURA wamenufaika katika nyanja mbalimbali ikiwemo ukuaji kiuchumi.
Mwenyekiti wa kikundi cha Tujipime ambacho kina wanachama 22 wanaoishi na VVU Manyanya Mkinga amesema tangu kikundi chao kiliposajiliwa mwaka 2019 wamefanikiwa kupata manufaa mbalimbali kupitia zabuni za TARURA wanazopata.
"Tuliona tukiungana hatuwezi kunyanyapaliwa wala kujinyanyapaa wenyewe hivyo kwa kazi hizi tunazopata za TARURA kwa kweli tumeweza kuboresha maisha yetu, licha ya kuishi na VVU tumefanikiwa kufanya kazi kwa ukamilfu, tunawashukuru sana TARURA kwa kutuwezesha kupata kazi." Amesema Mkinga.
Ametaja manufaa waliyoyapata tangu walipoanza kufanya kazi za TARURA mwaka 2020 ni pamoja na ujenzi wa nyumba za kuishi, ununuzi wa mashamba (parachichi na nyuki), kusomesha watoto pamoja na kujiunga na Bima ya Afya ya (NHIF).
Bw. Mkinga amesema kwa sasa wanaendelea na kazi ya ujenzi wa daraja mfuto (Vented Drift), kufyeka barabara Km.5, kujenga mitaro mita 5 na kinga maji kwenye mitaro katika barabara ya Mundindi-Ngogoma waliyoanza kujenga Septemba na wanatarajia kuikamilisha mwezi Oktoba mwaka huu.
Naye, Mwenyekiti wa kikundi cha Twili Lupangala Road Works Bw. Gutfred Mbilinyi amesema kwamba walianzisha kikundi hicho baada ya kuhamasishwa wa TARURA na wameweza kunufaika binafsi na wameweza kuanzisha miradi ya kikundi ikiwemo mashamba, ufugaji pamoja na ununuzi wa bodaboda tatu ambapo Malengo yao ya baadae ni kununua gari la kubeba mizigo.