Timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars leo Oktoba 10,2024 itashuka dimbani ugenini dhidi ya Congo DRC kweye mchezo wa kufuzu mashindano ya AFCON itakayofanyika nchini Morocco 2025. Stars itaingia kwenye mchezo huu ikichagizwa na urejeo wa Nahodha wa timu Mbwana Samatta ambaye alikosekana katika michezo miwili iliyopita ya timu ya taifa.
Michezo ya kufuzu AFCON 2025 nchini Morocco itachezwa siku ya leo Oktoba 10,2024 kwa michezo kupigwa mataifa tofauti barani Afrika. Mchezo unaosubiriwa na Watanzania ni ule utaokaozikutanisha timu ya taifa ya Congo DRC dhidi ya Tanzania, Taifa Stars kwenye uwanja wa Stade des Martyrs.
Kundi H linaongozwa na DRC yenye alama sita Stars inashiaka nafasi ya pili ikiwa imejikusanyia alama 4. Mchezo baina ya timu hizi mbili unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na matokeo ya siku za hivi karibuni pindi mataifa haya yanapokutana. Ambapo michezo mitatu ya hivi karibuni imetamatika kwa sare mbili na Tanzania imepoteza mchezo mmoja.
Mbwana Samatta anatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwenye mchezo huu kwa yale ambayo amewahi kuyafanya akiwa nchini Congo DRC alipokuwa anawatumikia klabu ya TP Mazembe ya Lubumbashi aliiwezesha timu hiyo kushinda ubingwa wa klabu bingwa Afrika mwaka 2015 alifanikiwa kumaliza mashindano akiwa mfungaji bora.
Tanzania itamkosa Abdulrazak Hamza aliye majeruhi, DRC itamkosa Yoane Wissa anayecheza Brentford ya Uingereza .Wachezaji Fiston Mayele na Henock Inonga Baka waliowahi kucheza ligi kuu Tanzania bara kwenye timu za Simba na Yanga wanaweza kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Mwalimu Sebastien Desabre.
Mchezo wa marudiano kuwania kufuzu AFCON 2025 itakayofanyika nchini Morocco kati ya Tanzania dhidi ya Congo DRC utachezwa Oktoba 15, 2024 nchini Tanzania kwenye dimba la Benjamini Mkapa.